Jinsi ya kufanya Biashara yako iwavutie Watu wengi

Wako wafanyabiashara wanaowahudumia wateja wao kama wanavyotaka na sio kama wateja wanavyotaka hii ni hatari sana inayoweza kukufukuzia wateja na kuathiri biashara.
"Mteja ni mfalme" ni msemo ambao umezoeleka na una maana kubwa, kuna wafanyabiashara wamekuwa wafalme kwenye biashara zao halafu wateja ndo watumwa unakuta wanaongea vibaya na wateja wao, anawakaripia na kuwagombeza wanasahau kuwa mteja hakosei ndio maana mteja anaitwa mfalme.
Siku zote mfanyabiashara anapaswa kuzingatia mahitaji ya wateja, matakwa yao pamoja na matamanio ya mteja ili kuweza kuwavutia wateja wengi na kulishinda soko la biashara lililojaa ushindani.
Wafanyabiashara waliogundua siri hiyo wamepiga hatua kubwa kiuchumi na kufanikiwa kuwateka wateja wengi na kutengeneza faida kubwa katika biashara zao kutoa huduma bora kwa wateja inayowafanya wateja waridhike na wafurahie huduma ama bidhaa wanazouziwa. Matokeo yake wameliteka soko kwa ubora wa bidhaa zao, ubunifu na huduma bora kwa wateja wao.
Tumeshuhudia wafanyabiasha wengi wakifanya biashara kimazoea miaka nenda rudi bila ya kuwa na maboresho,ubunifu.Wengine wanawaona wateja kama wasumbuaji hawawajali,wanatumia kauli mbaya, hawayafahamu kiundani matamanio wala mahitajio ya wateja na namna ya kutoa huduma bora kwa mteja.
Kwa ujumla hawatumii kanuni za kisayansi za kufanya biashara wengi wao mambo huwaendea mrama na kujikuta wakipata hasara mara kwa mara.
Yapo mambo matano unayoweza kuyatumia kuwavutia wateja katika biashara yako na kukufanya ufanikiwe katika biashara, mambo hayo ni pamoja na;
Lugha nzuri inayoambatana na tabasamu. Hiki ni kivutio kikubwa cha wateja wanapokuja kwenye biashara yako na kitamfanya arudi ama aje mara kwa mara ndio maana hata wewe msomaji unachagua kutumia sehemu yenye huduma inayokuridhisha, kuna watu wamefanikiwa kibiashara na kimaisha kutokana na kauli zao nzuri.Hivyo utakubaliana nami kuwa "kauli ni mali" na "ofisi ya kwanza ya mtu ni mdomo wake".
Tabasamu na kauli nzuri humfanya mteja kumuona mfanyabiashara kama rafiki yake na kufanya urahisi wa biashara yako.
Mfano unaweza kwenda sehemu watu wanauza chakula mhudumu amenuna au anaongea vibaya. Hata mafundi wengi wametawaliwa na uongo na ahadi wasizozitimiza,haya ni mambo yanayoweza kumkimbiza mteja.
Kama unavyojua mteja mmoja akihudumiwa vibaya huwaaambia wenzake 15, hao 15 huwaambia wenzao kila mmoja watu 6. Baada ya Muda wateja wanapungua ghafla unakosa kabisa na kuanza kufikiri kuwa umelogwa unaanza kukimbilia kwa waganga na wakati umejiloga wewe mwenyewe na ulimi wako. Lugha nzuri inamfanya mhudumu avutie wateja na kuonekana vizuri.
Mazingira masafi na bora ni jambo la pili linalowavutia wateja na kufanikisha bishara,mazingira safi na bora ni jinsi biashara yako inavyoonekana kwa nje mpaka ndani, vifaa vyake na vifaa vinavyotumika kama nyezo.
Mfano unakuta mgahawa mbele yake kuna dibwi la maji machafu, vifaa kama jiko, sahani, bakuli ni vichafu na chakavu, hali kama hii haimvutii mteja.
Jambo la tatu Muhudumu awe msafi unakuta muhudumu anahudumia ana plasta mkononi, amevaa kanda mbili, nguo chafu yaani amevaa zile sare nyeupe za wapishi zimechafuka, zimebadilika rangi na kuwa kahawia.
Mteja anategemea kumkuta mhudumu msafi vitu hivyo vinawakera wateja hata kabla ya kuhudumiwa. Mteja anategemea kukutana na mhudumu msafi, mfano wahudumu wa ndege.
Mteja anatarajia kuhudumiwa kwa wakati. Mteja akifika eneo husika, muhudumu amfuate na kumhoji angependa ahudumiwe nini? Baadhi ya sehemu nyingine si ajabu kukaa muda mrefu bila kupata mtu wa kukuhudumia na wahudumu wapo.
Hakikisha unampa mteja zaidi ya kile alichotarajia kupata kutoka kwako nina maana kumpa mteja kitu cha ziada Mmano kwenye mgahawa mtu akinunua chakula unamuongezea vitu kama matunda, kachumbari na maji bila kumtoza gharama, wateja wengi ni watu wa kusema sema kauli zao zina matokeo hasi ama chanya kutokana na ulivyomhudumia.
Sehemu nyingine ukienda hotelini kabla ya kuhudumiwa unapewa juisi ambayo hauilipii lakini madhara ya juisi hiyo ni makubwa. Ni rahisi kwa wateja kuwa waaminifu kwa biashara zenye mazingira kama hayo.
Wiki ijayo tutajifunza aina za wateja na jinsi ya kuwahudumia ili kuweza kupata wateja wengi na kufanikiwa kuwateka kwa wingi na kufanikiwa kibiashara.
No comments:
Post a Comment